Ebola na Marburg: Baada ya Kusafiri

Ukurasa huu unatoa taarifa kwa watu wanaosafiri kwenda Marekani kutoka eneo lenye mlipuko wa Ebola au Marburg.

  • Kwa sasa hakuna milipuko ya Ebola ao Marburg inayoendelea.

Ebola na Marburg huenea kupitia kugusana moja kwa moja na damu au maji maji ya mwili (mate, shahawa, jasho, kinyesi, matapiko, na mengineyo) ya mtu ambaye ni mgonjwa au amekufa kutokana na Ebola au Marburg. Unaweza pia kupata Marburg kwa kugusana na aina ya popo wa matunda wanaopatikana Afrika au maji maji ya mwili wa popo.

Iwapo umesafiri kutoka eneo lililo na mlipuko, zingatia afya yako kwa siku 21 baada ya kuondoka eneo hilo la mlipuko. Zingatia:

  • Homa (100.4°F/38°C au zaidi) au kuhisi kama una homa
  • Kuumwa na kichwa au maumivu mwilini
  • Upele
  • Udhaifu au uchovu
  • Maumivu ya koo
  • Kuhara
  • Kutapika
  • Maumivu kwenye tumbo
  • Kuvuja damu au michubuko isiyoelezeka

Pima joto lako ukihisi kuwa mgonjwa.

Mambo ya Kufanya Ukiugua Baada ya Kusafiri

Ukipata dalili za Ebola au Marburg

  • Jitenge na wengine (usitangamane).
  • Piga simu kwa idara ya afya ya eneo lako ili upate ushauri kuhusu huduma ya matibabu. Eleza idara ya afya kuhusu safari yako ya hivi majuzi kutoka nchi yenye mlipuko wa Ebola au Marburg na dalili zako ili waweze kutambua kituo bora zaidi cha huduma ya afya ambacho unaweza kwenda. Idara ya afya inaweza kusaidia kituo kujiandaa kukupa huduma na kuchukua tahadhari zozote zinazohitajika.
  • Ikiwa huwezi kufikia idara yako ya afya, piga simu kwa mtoa huduma ya afya. Waambie dalili zako na kwamba hivi majuzi ulikuwa katika nchi iliyo na mlipuko wa Ebola au Marburg. Kupiga simu kabla ya kwenda kwenye kituo cha afya husaidia kituo kujiandaa kwa ajili ya kuwasili kwako, ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na idara ya afya na kuchukua tahadhari zozote zinazohitajika.
  • Usisafiri ukiwa mgonjwa. Safiri tu wakati umeidhinishwa na daktari au afisa wa afya.